Saturday, April 16, 2011

Mtemi Fundikira III ( Abdallah Said)

Mtemi Fundikira(III)Abdallah Said.(1957-1962).1957-2007

Hili ni kaburi la Mtemi Fundikira III, katika Ikulu ya Itetemya.

Huyu alikuwa Mtemi wa 19  wa Unyanyembe. Utawala wake ulidumu kwa miaka 5 kuanzia mwaka 1957 mpaka 1962. Baada ya Tanganyika kupata uhuru 1961 ndipo Mwalimu Nyerere alipofuta utemi wa dola rasmi mwaka 1962. Mtemi huyu ana historia kubwa sana katika nchi ya Tanganyika pamoja na kuwa haipewi nafasi katika vitabu vya historia na kwingineko. Baada ya hapo alibaki kuwa Mtemi wa jadi tu na asiye na nguvu yeyote ya kuendesha serikali mpaka alipofariki usingizini nyumbani kwake Mwanza Road, Tabora mnamo tarehe 8/8/2007.
Historia zaidi kuhushu Mtemi Fundikira III zitafuata... 
Hapa akiwa nje ya Ikulu ya Itetemia 1957.
Ikulu yake iliyopo Itetemia

Mtemi Fundikira III akitawalishwa 1957

Friday, April 15, 2011

Mtemi Fundikira II (Nassor Said) kimala masasi!

Mtemi Fundikira II( Nassor Said)

Dirisha la chumba alichojipigia risasi Mtemi Fundikira III 1957.
Alitawala kuanzia mwaka 1948 mpaka 1957, utawala wake ulidumu kwa miaka 9. Mtemi huyu alipotawala aliweka mikakati ya kukomesha wizi wa mifugo, aliwatangazia wezi wote wajisalimishe kabla hawajatafutwa na kukamatwa, na kweli wezi wote wa mifugo walijisalimisha na wizi wa mifugo hasa ng'ombe ukaisha kabisa katika nchi ya Unyanyembe na jambo hili lilipelekea akatunukiwa medali ya heshima iitwayo ORDER OF THE BRITISH EMPIRE (OBE) na Malkia Elizabeth II katika Ikulu yake Buckingham Palace mjini London. Hii ni heshima kubwa sana ambayo si watanzania wengi wamewahi tunukiwa medali hiyo. Baadae mwaka 1957 ulitokea ubadhirifu wa pesa za serikali katika nchi yake Unyanyembe na ilikuwa dhahiri yeye ndiye kazila, askari wa kikoloni (Waingereza) walipotaka kumkamata akajifungia chumbani mwake na kujipiga risasi na kufa.
Mtemi Fundikira II (Nassor Said) Order of the British Empire.

Mtemi Mkasiwa ( Ilagila)

Mtemi Mkasiwa alitawala kuanzia mwaka 1932 mpaka 1948 na utawala wake kudumu miaka 16. Huyu hakutaka kutawala ila alilazimishwa na ndio sababu ya kuitwa Mkasiwa. Pia huyu alikuwa ni mtu wa aina yake, kwani yeye alikuwa binti ya Mtemi kisha akaolewa na Mtemi Mkwawa na baadae akawa Mtemi wa Unyanyembe. 

Mtemi Kiyungi Mwana Isike

Huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike mwana Kiyungi alitawala kuanzia mwaka 1928 mpaka 1932.

Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said)

Hili ndilo kaburi la  Mtemi Swetu(Said) Fundikira alizikwa hapo mwaka 1961.
Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said) huyu alikuwa Mtemi maarufu sana katika nchi ya Tanganyika, alitawala kuanzia mwaka 1917 mpaka 1927. Alifanikiwa kuwashawishi watemi wengine  wa kanda ya magharibi kuchanga pesa, mifugo na mali nyingine ili

Mtemi Said (sultan said) Fundikira 1956
Sultan Said Fundikira na Mw Nyerere 1956

Mzee Ramadhani said Fundikira

kupata pesa za kujenga shule mbili za Tabora Boys na Tabora Girls. Na yeye akatoa ardhi ya kujenga shule hizo kwa kuwa eneo hilo lilikuwa chini ya himaya ya Ikulu ya Unyanyembe. Vile vile Mtemi Said alikuwa mkarimu mno kiasi kwamba mtu akiunguliwa na nyumba yeye alimjengea nyumba mpya na kumpa chakula cha kumtosha kwa mwaka mzima. Na kila mwisho wa mwezi alipokuwa akitoka Bomani kuchukua mshahara wake ulikuwa ni shilingi 4000, ambazo hata Gavana wa Kiingereza Bw Donald Cameron alipata kiasi hicho pia. Watu wenye shida walijpanga katika barabara ya Luhanzali wakimtolea shida zao naye aliwasaidia kwa kuwapa pesa za mshahara wake na hata alipofika Ikulu Itetemia alijikuta kuwa ameishiwa pesa zote.  

Yeye aliondolewa madarakani na wakoloni wa kiingereza baada ya kuwa hapeleki serikalini kodi aliyotoza wananchi, inasadikika alitumia pesa hizo kusaidia masikini. Hivyo kwa heshima na upendo aliyokuwa nao kwa wananchi wake wakoloni wa Kiingereza walilazimika wasimfunge jela ila walimuondosha Itetemia na kiti chake akakitwaa Mtemi Kiyungi II huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike Mwana Kiyungi. 

Sultan Said alijaaliwa kupata watoto 57 ambao miongoni mwao ndio hawa kina marehemu Chief Abdallah Fundikira, Ramadhani Mlawila (Baba yangu), Kagori biti Said (Mama yake Samuel Sitta) na wengi wengine.Na mpaka sasa katika watoto hao 57 wamebaki wanawake watatu Kagori na Ndisha na mwanamume mmoja Ramadhani Mlawila (87) aliyepata kuwa waziri mkuu katika ofisi ya Mtemi Fundikira III pia aliwahi kukaimu Utemi wakati Mtemi Abdallah (Fundikira III) alipoingia serikalini.

Nyumba hii ilitumiwa na waziri mkuu Mlawila 1957-64

Ninavyofikiri mimi Sultan Said ndiye aliyeuingiza ukoo huu wa Fundikira katika dini ya ki Islam, kwa kuwa yeye alisomea Zanzibar ambako dini hiyo ilishasambaa huko. Bila shaka aliporudi bara ndipo akaja na dini hiyo ambayo mpaka sasa ndiyo imekua dini ya Ukoo huu. Na hakuna ushahidi kama ukoo huu uliwahi kuwa waumini wa dini yeyote kabla miaka ya 1900. Hivyo basi inaelekea ukoo huu uliabudu mizimu kama ilivyo desturi ya wa Afrika.
Sultan Said aliishi katika nyumba hii baada ya kuruhusiwa kurudi Itetemia

Mtemi Kalunde Mwana Gumadi

Hili ndilo kaburi la Mtemi Kalunde Mwana Gumadi alitawala 1896-1917


Alitawala baada ya Mtemi Nyamso kufariki mwaka 1896, naye alitawala kuanzia mwaka huo huo mpaka mwaka 1917. Mtemi huyu alikuwa mwadilifu sana na alipenda kusaidia watu kutatua matatizo yao, alikuwa akiamka saa 12 asubuhi na kupita kwenye maofisi kukagua kazi mbali mbali na pia kuona kama maafisa wake wamekwenda maofisini mwao kusikiliza shida za wananchi. Na inapofika mchana chakula kinapokuwa tayari alikuwa akipiga kengele ili mtu yeyote aliyepita hapo aende akale, kwa kifupi alikuwa mtu mkarimu sana. Ilipofika mwaka 1917 alifariki.

Mtemi Nyanso

Huyu baada ya Wajerumani kumuondoa Mtemi Isike ndipo akatawala yeye kuanzia mwaka 1893 mpaka mwaka 1896 ambapo aliugua na hatimaye kufa.
Stori zaidi kuhusu utawala wa Mtemi Nyanso ambaye ndiye alinusurika kuuawa na Mtemi Isike zitafuata