Saturday, April 16, 2011

Mtemi Fundikira III ( Abdallah Said)

Mtemi Fundikira(III)Abdallah Said.(1957-1962).1957-2007

Hili ni kaburi la Mtemi Fundikira III, katika Ikulu ya Itetemya.

Huyu alikuwa Mtemi wa 19  wa Unyanyembe. Utawala wake ulidumu kwa miaka 5 kuanzia mwaka 1957 mpaka 1962. Baada ya Tanganyika kupata uhuru 1961 ndipo Mwalimu Nyerere alipofuta utemi wa dola rasmi mwaka 1962. Mtemi huyu ana historia kubwa sana katika nchi ya Tanganyika pamoja na kuwa haipewi nafasi katika vitabu vya historia na kwingineko. Baada ya hapo alibaki kuwa Mtemi wa jadi tu na asiye na nguvu yeyote ya kuendesha serikali mpaka alipofariki usingizini nyumbani kwake Mwanza Road, Tabora mnamo tarehe 8/8/2007.
Historia zaidi kuhushu Mtemi Fundikira III zitafuata... 
Hapa akiwa nje ya Ikulu ya Itetemia 1957.
Ikulu yake iliyopo Itetemia

Mtemi Fundikira III akitawalishwa 1957

Friday, April 15, 2011

Mtemi Fundikira II (Nassor Said) kimala masasi!

Mtemi Fundikira II( Nassor Said)

Dirisha la chumba alichojipigia risasi Mtemi Fundikira III 1957.
Alitawala kuanzia mwaka 1948 mpaka 1957, utawala wake ulidumu kwa miaka 9. Mtemi huyu alipotawala aliweka mikakati ya kukomesha wizi wa mifugo, aliwatangazia wezi wote wajisalimishe kabla hawajatafutwa na kukamatwa, na kweli wezi wote wa mifugo walijisalimisha na wizi wa mifugo hasa ng'ombe ukaisha kabisa katika nchi ya Unyanyembe na jambo hili lilipelekea akatunukiwa medali ya heshima iitwayo ORDER OF THE BRITISH EMPIRE (OBE) na Malkia Elizabeth II katika Ikulu yake Buckingham Palace mjini London. Hii ni heshima kubwa sana ambayo si watanzania wengi wamewahi tunukiwa medali hiyo. Baadae mwaka 1957 ulitokea ubadhirifu wa pesa za serikali katika nchi yake Unyanyembe na ilikuwa dhahiri yeye ndiye kazila, askari wa kikoloni (Waingereza) walipotaka kumkamata akajifungia chumbani mwake na kujipiga risasi na kufa.
Mtemi Fundikira II (Nassor Said) Order of the British Empire.

Mtemi Mkasiwa ( Ilagila)

Mtemi Mkasiwa alitawala kuanzia mwaka 1932 mpaka 1948 na utawala wake kudumu miaka 16. Huyu hakutaka kutawala ila alilazimishwa na ndio sababu ya kuitwa Mkasiwa. Pia huyu alikuwa ni mtu wa aina yake, kwani yeye alikuwa binti ya Mtemi kisha akaolewa na Mtemi Mkwawa na baadae akawa Mtemi wa Unyanyembe. 

Mtemi Kiyungi Mwana Isike

Huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike mwana Kiyungi alitawala kuanzia mwaka 1928 mpaka 1932.

Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said)

Hili ndilo kaburi la  Mtemi Swetu(Said) Fundikira alizikwa hapo mwaka 1961.
Mtemi Saidi Fundikira (Sultan Said) huyu alikuwa Mtemi maarufu sana katika nchi ya Tanganyika, alitawala kuanzia mwaka 1917 mpaka 1927. Alifanikiwa kuwashawishi watemi wengine  wa kanda ya magharibi kuchanga pesa, mifugo na mali nyingine ili

Mtemi Said (sultan said) Fundikira 1956
Sultan Said Fundikira na Mw Nyerere 1956

Mzee Ramadhani said Fundikira

kupata pesa za kujenga shule mbili za Tabora Boys na Tabora Girls. Na yeye akatoa ardhi ya kujenga shule hizo kwa kuwa eneo hilo lilikuwa chini ya himaya ya Ikulu ya Unyanyembe. Vile vile Mtemi Said alikuwa mkarimu mno kiasi kwamba mtu akiunguliwa na nyumba yeye alimjengea nyumba mpya na kumpa chakula cha kumtosha kwa mwaka mzima. Na kila mwisho wa mwezi alipokuwa akitoka Bomani kuchukua mshahara wake ulikuwa ni shilingi 4000, ambazo hata Gavana wa Kiingereza Bw Donald Cameron alipata kiasi hicho pia. Watu wenye shida walijpanga katika barabara ya Luhanzali wakimtolea shida zao naye aliwasaidia kwa kuwapa pesa za mshahara wake na hata alipofika Ikulu Itetemia alijikuta kuwa ameishiwa pesa zote.  

Yeye aliondolewa madarakani na wakoloni wa kiingereza baada ya kuwa hapeleki serikalini kodi aliyotoza wananchi, inasadikika alitumia pesa hizo kusaidia masikini. Hivyo kwa heshima na upendo aliyokuwa nao kwa wananchi wake wakoloni wa Kiingereza walilazimika wasimfunge jela ila walimuondosha Itetemia na kiti chake akakitwaa Mtemi Kiyungi II huyu alikuwa mtoto wa Mtemi Isike Mwana Kiyungi. 

Sultan Said alijaaliwa kupata watoto 57 ambao miongoni mwao ndio hawa kina marehemu Chief Abdallah Fundikira, Ramadhani Mlawila (Baba yangu), Kagori biti Said (Mama yake Samuel Sitta) na wengi wengine.Na mpaka sasa katika watoto hao 57 wamebaki wanawake watatu Kagori na Ndisha na mwanamume mmoja Ramadhani Mlawila (87) aliyepata kuwa waziri mkuu katika ofisi ya Mtemi Fundikira III pia aliwahi kukaimu Utemi wakati Mtemi Abdallah (Fundikira III) alipoingia serikalini.

Nyumba hii ilitumiwa na waziri mkuu Mlawila 1957-64

Ninavyofikiri mimi Sultan Said ndiye aliyeuingiza ukoo huu wa Fundikira katika dini ya ki Islam, kwa kuwa yeye alisomea Zanzibar ambako dini hiyo ilishasambaa huko. Bila shaka aliporudi bara ndipo akaja na dini hiyo ambayo mpaka sasa ndiyo imekua dini ya Ukoo huu. Na hakuna ushahidi kama ukoo huu uliwahi kuwa waumini wa dini yeyote kabla miaka ya 1900. Hivyo basi inaelekea ukoo huu uliabudu mizimu kama ilivyo desturi ya wa Afrika.
Sultan Said aliishi katika nyumba hii baada ya kuruhusiwa kurudi Itetemia

Mtemi Kalunde Mwana Gumadi

Hili ndilo kaburi la Mtemi Kalunde Mwana Gumadi alitawala 1896-1917


Alitawala baada ya Mtemi Nyamso kufariki mwaka 1896, naye alitawala kuanzia mwaka huo huo mpaka mwaka 1917. Mtemi huyu alikuwa mwadilifu sana na alipenda kusaidia watu kutatua matatizo yao, alikuwa akiamka saa 12 asubuhi na kupita kwenye maofisi kukagua kazi mbali mbali na pia kuona kama maafisa wake wamekwenda maofisini mwao kusikiliza shida za wananchi. Na inapofika mchana chakula kinapokuwa tayari alikuwa akipiga kengele ili mtu yeyote aliyepita hapo aende akale, kwa kifupi alikuwa mtu mkarimu sana. Ilipofika mwaka 1917 alifariki.

Mtemi Nyanso

Huyu baada ya Wajerumani kumuondoa Mtemi Isike ndipo akatawala yeye kuanzia mwaka 1893 mpaka mwaka 1896 ambapo aliugua na hatimaye kufa.
Stori zaidi kuhusu utawala wa Mtemi Nyanso ambaye ndiye alinusurika kuuawa na Mtemi Isike zitafuata

Thursday, April 14, 2011

Mtemi Isike mwana Kiyungi

Hili lilikuwa lango la ngome ya Mtemi Isike mwana Kiyungi ikiitwa Isyinula 1893, Wajerumani walishindwa kuipenya kwa miaka mitano ya vita.
Alitawala kuanzia mwaka 1885, yeye alikuwa mtoto wa Mt Kiyungi kama alivyokuwa Swetu Kalonga ambaye aliwaua nduguze wa tumbo la Fundikira ili tumbo la Kiyungi litawale kwa nafasi bila kuingiliwa na tumbo la Fundikira.  Swetu Kalonga kwa mara nyingine tena alimshawishi kaka yake Isike wawaue tumbo la Fundikira ili wajihakikishie utawala utabaki katika tumbo lao la Kiyungi. Mt Isike alikubali ndipo akapanga mipango na wazee (wanikulu) wamwite Nyanso  Bint Fundikira toka kwake Ndevelwa na akifika Ikulu ya Itetemya wamuue, wakachimba shimo na wakachomeka mikuki na miti yenye ncha kali ndani yake kisha wakaliwekea fito nyembamba kwa juu na kulifunika kwa majani wakaweka kiti juu yake ili atakapokuja  Nyanso wamkaribishe akae katika kiti hicho atumbukia shimoni ili mikuki imchome mpaka afe.. Kwa bahati wakati wakipanga mipango hiyo nje alikuwepo mtoto wa kaka yake Ifuma akiitwa Kipini aliwasikia yote waliyopanga , Kipini yeye alikuwa mwehu ndipo alipokuja shangazi yake Nyanso kuitikia wito wa Mt Isike  yeye Kipini alianza kumwambia Nyanso "sengi ngenewikale hanahohisumbu wasimbagaliina watulaga na masonga walikova wakuwulage, ngeneugeme kwikalanaho" ndipo Nyanso na wazee wakabaki wanashangaa mlinzi mmoja wa Nyanso akaenda akakiondoa kile kiti akakikalia yeye kwanza , akasimama akaanza kuchoma choma na mkuki pale palipokuwa kiti akaona mchanga unatumbukia ndani ya shimo ndipo Nyanso akamuuliza Mt Isike "nasumulakii mbona uliova kuniwulaga? Mt Isike akawa hana jibu. Nyanso akakasirika sana akaamua kuondoka na kurudi Ndevelwe, Kisha akaenda bomani kwa DC akaomba msaada wa kumpiga vita Isike ili wamuondoe kwenye utawala na huo ulikuwa mwaka 1889. Dc akamwita kamanda wa majeshi ya Ujerumani aitwaye Bw Sakarani(Von Prince) na kumpa kazi ya kumuondoa Isike katika utawala. Von Prince akaendesha vita ya kumpiga  Mt Isike, vita vikapiganwa kwa miaka minne majeshi ya Ujerumani yalishindwa kumuondoa Mt Isike. Ndipo Sakarani akatuma ujumbe  kwa Mtemi Isike kumwambia vita isimame. Mtemi Isike alikubali na vita ikasimama. Kumbe bwana Sakarani ( von Prince) alikuwa anataka kuichunguza Ikulu ya Itetemia na uimara wa jeshi la Unyanyembe ndipo akaamua kuomba msaada wa waarabukwa kiongozi wa waarabu akiitwa Msolopa akakubali kumpeleka Ikulu ya Itetemya kama vile kumpa pole kwa vita ya kupambana na Wajerumani . Von Prince akaenda kwihara  akavaa nguo za kiarabu, kilemba na kanzu wakaondoka kwenda Itetemya wakiwa jumla watu wanne .Walipofika Mt Isike akawapokea baada ya kunywa chai akaomba awatembeze Ikulu ili wamsaidie kuitengeneza kwa kuwa ilipigwa mizinga mitatu lakini haikubomoka.Baada ya kuwatembeza wakala chakula cha mchana na wakaaga wakaondoka.

Baada ya kuisoma Ikulu ya Mtemi Isike, Von Prince akaagiza silaha mpya na zenye nguvu na za kisasa kwa wakati huo ili aivamie tena Ikulu hiyo. Ilipofika tarehe 22/2/1893 silaha ziliwasili
na majeshi ya ujerumani yalivamia tena Ikulu ya Itetemya , walipigana kwa takriban mwaka mmoja hivi majeshi ya Mtemi Isike yakashindwa vita, ndipo Mtemi Isike akakamatwa na walipotaka kumpeleka bomani akakataa Von prince akamwambia basi utanyongwa Mtemi isike akasema bora ndipo akamnyang'anya kamba mmoja wa askari akajifunga shingoni akapanda katika kiti akajinyonga.

Mtemi Kiyungi II

Mtemi Kiyungi alitawala kuanzia mwaka 1864, alikuwa mtoto wa Msagata ndiye aliyezaliwa Uwemba na mama yake alikuwa Muwemba (Zambia) Mara baada ya kutwaa madaraka ya utemi wa Unyanyembe, Mirambo akavamia Unyanyembe zaidi ya mara tano lakini mara hizo zote Mirambo alishindwa vita.


Mtemi  Mirambo
Mtemi Mirambo
 Na kipindi chote cha utawala wake aliandamwa na maneno maneno sana hasa toka upande wa Fundikira uliokuwa ukisema kuwa Kalunde amekosea kumtawalisha Kiyungi  maana hawakua na uhakika kama Kiyungi kweli alikuwa mtoto wa Msagata kweli au vipi! Baada ya maneno hayo kupamba moto, mtoto wa Mtemi Kiyungi aliyeitwa Swetu Kalonga akaenda kumshawishi baba yake kuwa ni bora wawaue kina Fundikira wote ili wao tumbo la Kiyungi waweze kuyawala kwa raha bila shutuma toka tumbo la Fundikira, lakini baba yake alikataa wazo hilo na alimfokea sana Swetu Kalonga na kumwambia "Tena usirudie siku nyingine kunambia maneno kama hayo yaani mimi niwaue bwana zangu walionitoa Uwemba na kunipa kiti cha utawala, wewe una akili kweli wewe? Tena ukome kama ulivyokoma ziwa la mama yako, mimi si mtu mjinga mjinga kama unavyofikiria" Swetu akaondoka lakini akiwa na maamuzi yake kichwani baada ya miezi sita Swetu akaanza kuwaua mwenyewe tumbo la Fundikira. Mtu wa kwanza kumuua alikuwa  Mantumanha na wa pili akawa Kaveve na wengine wengi tu akawaua.Baada ya miaka miwili Mtemi Kiyungi akaamua kumuunga mkono
mwanawe Swetu kuwaua tumbo la Fundikira na akaamrisha Iguli,Msokoni na Kulwa wauawe. Habari hizo zikamfikia Mwanangwa Kalunde binti wa Mtemi Fundikira aliyekuwa akiishi Ndevelwa alikuwa ameolewa na mwarabu mmoja akiitwa  Mohamed bin Hemed el Murjebi huyu ni baba wa Tip Tip. Baada ya Kalunde kupata habari hizo alikasirika sana akapanga kwenda kumtukana Mtemi Kiyungi. Siku ilipofika akaamka saa 11 alfajiri akatoka na walinzi wake na baadhi ya wazee kuelekea Ietemya
akafika pale Itetemya saa 12 asubuhi akamkuta Mtemi Kiyungi ndio kwanza ameamka amekaa katika chake cha utawala akiwa anasubiri watu waende kumsabahi. Kalunde alijifunga nguo tumboni na kuacha maziwa wazi akainua mkono wake wa kushoto na kukinga macho kama anaye kinga jua , akamsogelea Mtemi Kiyungi na kumwambia " wagerahe munuyu mnyaluwemba" Mt Kiyungi akajibu "neneaha mayuu" Kalunde akaanza kumtukana " wewe mnyaluwemba na kupisumbi ulamalawana wansi atiwuli wamuhulaga Mantumana wamuhulaga na Kaveve, Iguli na Msokoni izahangi wamuhulaga Kulwa alumunihuyu Kulwa wasumlakii? Mt Kiyungi akaanguka chini  ya miguu ya Kalunde huku akisema napelage mayuu napelage mayuu napelage mayuu Kalunde akamwambia "ukome kama ulivyokoma kuwaua tumbo la Fundikira kisha kisha akamsonya syoooo akaondoka na kurudi kwake  Ndevelwa. Baada ya hapo Mt Kiyungi akaacha kabisa kuwaua tumbo la Fundikira mpaka alipokufa mwaka 1885.

Mtemi Mnwasele

Mtemi Isale aka Fundikira kabla ya kufariki alimpendekeza Matandula Mdaki amabye alikuwa ni mpwa wake mtoto wa dada yake Msilu Swetu awe mrithi wake kiti cha utemi. Lakini Mnwasele alipinga Matandula kuwa Mtemi wa Unyanyembe kwa kuwa Matandula Mdaki kwao ni Kigwa na kuna utemi kule, je akifa mtemi wa kwao atatawala nani? au ataenda kutawala yeye tena?  Wazo hilo la Mnwasele wazee waliliunga mkono  na baada ya Mtemi Isale Fundikira kufariki , Mnwasele akaanza kutoa vitisho kwa wazee, kuwa kama wangemtwalisha Matandula Mdaki angemchoma mkuki palepale pa kutawalishia watemi. Basi wazee wakaogopa na kwa kuwa Mnwasele alikuwa shujaa mkubwa katika medani ya vita hivyo wakaamua wamtawalishe yeye na akawa Mtemi wa 10 wa Unyanyembe mnamo mwaka 1859 na utawala wake ulidumu kwa miaka mitano tu.

Mtemi Isale aka Fundikira (I)

MTEMI ISALE aka FUNDIKIRA

Alikuwa Mtemi wa pili kutawala katika Ikulu ya Itetemya, alitawala mpaka akazeeka kiasi kwamba wabaya wake na watu wasiompenda wakawa wanamafanyia njama ili wamuue ili atawale mtu mwingine.

CHANZO CHA JINA FUNDIKIRA

Miongoni mwa watu waliomchoka Mtemi Isale alikuwa ndugu yake mmoja akiitwa Mkelemi, huyu Mkelemi alikuwa mtoto wa Kiwisuka mwana Sambwe, yeye alikuwa akiishi eneo ambalo kwa sasa linaitwa Tuli. Akawa anazungumza wazi wazi "Huyu Mtemi mbona anachelewa kufa, na sisi tutatawala lini?, akaongeza ipo siku nitaenda kumsabahi na ndipo nitamchoma mkuki afe"

Habari hizo zikaenea mpaka zikamfikia mwenyewe Mtemi Isale. Mtemi akaona bora asipuuze, akawaita wazee wanikulu wazijadili zile habari, wamchukulie hatua gani huyo Mkelemi. Baada ya mjadala mrefu wakakubaliana wampelekee  jeshi likampige afe. Wakati wanapanga mikakati hiyo ya kumpelekea jeshi alikuwepo mtoto wa Mtemi Mmanywa, yeye alipinga wazo la kumpelekea jeshi mtu mmoja akawaambia "niachieni mimi nitamuua kwa mkono wangu"

Wazee na Mtemi wakakubali wakamuachia yeye akamuue Mkelemi. Nkosi alikuwa akiishi Migwenhwe hivyo akatuma ujumbe kwa Mkelemi kuwa anamualika aende kwake akamtembelee. Mkelemi alikubali na ilipofika siku hiyo Nkosi akachimba shimo la duara na ndani ya shimo akachomeka mikuki na miti yenye ncha kali huku ikiwa imeangalia juu. Akachukuaa miti akaitandika juu ya shimo lile akatandaza majani kisha akafunika na udongo na juu yake akaweka kiti. Ilipofika saa 5 hivi Mkelemi akawasili kwa Nkosi, akampokea na kumkaribisha katika kiti alichokiandaa na Mkelemi alipokaa tu akatumbukia na kuchomwa na mikuki na miti iliyokuwamo mle shimoni akawa analia huku akisema "Nkosi wambulaga"  akimaanisha Nkosi umeniua. Nkosi akamjibu "Nkali nene wakuwala uwayawako msava veve ulikova kumwulaga Mtemi wakusumla kinani? akimaamisha Nkosi akaona Mkelemi anachelewa kufa akachomoa mkuki akainama na kumchoma Mkelemi lakini kumbe Mkelemi nae alichomoa kisu na kunyoosha mkono juu kile kisu kikamchoma Nkosi tumboni na yeye akaangukia humo shimoni akafa kwa utumbo wake ulimwagika kutokana na jeraha la kisu cha Mkelemi. Mke wa Nkosi akaanguka chini na kuanza kulia na kupiga ukelele uuuwi winulaga akimaanisha jamani wamemuua. Watu wakaja wakawatoa toka mle shimoni. Nkosi akawa ashakufa lakini Mkelemi akawa bado hajafa. wakawabeba kwenye machela mbili wakawapeleka Ikulu kwa Mtemi. Wakamsimulia Mtemi yaliyotokea, Mtemi akawaambia "huyu Mkelemi mpelekeni kwake na huyu Nkosi tumzike.

Watu wakambeba wakimrudisha nyumbani kwake njiani huku akivuja sana damu Mkelemi akawaambia "mwemweye ntulinasuhe, wale wtu wakamshusha chini akasema " mpagi minzi nang'we"
wakafuata maji kwenye malambo wakampa akanywa alipomaliza kunywa akafa.Wakabeba maiti mpaka nyumbani kwake, kesho yake wakazika, tokea siku hiyo eneo hilo likaitwa Tuli mpaka leo eneo hilo linaitwa hivyo.

Baada ya siku 40  Mtemi Isale akawaambia watu leteni nguo za Mkelemi na Nkosi walipoleta nguo zao akawaambia sikilizeni hizi nguo nitazichukua mimi kwa sababu hawa Mkelemi na Nkosi wameuana kwa ajili yangu akasema kwa kinyamwezi navakundikila Nkosi na Mkelemi akimaanisha nawafunika Mkelemi na Nkosi. Tangu siku hiyo mtemi akawa anaitwa ikundikila na jina hilo likabaki mpaka hii leo na ndio asili ya jina la Fundikira.

Wednesday, April 13, 2011

Tumbo la Kiyungi (Nsamama)

Mtemi Kiyungi baba yake aliitwa Msagata Mwana Mgalula, Kiyungi alizaliwa Uwemba (Zambia) .Wakati wa utawala wa Mtemi Fundikira ( I ) Msagata kazi yake ilikuwa kuwinda Tembo hivyo alikwenda Uwenba kuwinda Tembo, katika harakati zake zauwindaji huko Uwemba akampachika mimba binti ya Mtemi wa huko, kwa kuwa lilikuwa ni kosa kubwa  ilimbidi atoroke arudi nyumbani Unyanyembe, baada ya mwaka hivi zikaja habari kuwa binti ya Mtemi kajifungua mtoto wa kiume. Msagata akamwambia baba yake mdogo Mtemi Fundikira habari zile, Mtemi Fundikira akamwambia nenda pwani kauze meno ya Tembo ukirudi nitakupa mali ukamgomboe mwanao.

Msagata akaenda pwani kuuza meno ya tembo wakati anarudi akapata ugonjwa wa ndui akafa njiani. Ndipo Mtemi Fundikira  akamtuma mdogo wake Msagata aliyeitwa Msyama achukue mali aende akamgomboe yule mtoto kule Uwemba. Msyama akaenda kumgomboa akarudi na mtoto pamoja na mama yake, huko Uwemba mtoto yule alipewa jina la Nsamama. Na huku Nsyepa akapewa jina la Kiyungi. Mtemi Fundikira akafurahi sana kuona yule mtoto ameletwa, wakapiga lugaya pakachinjwa ng'ombe sherehe zilifanyika kwa siku 7, watu walikula na kucheza ngoma siku hizo zote.

Huyu Nsamama (Kiyungi) Baadae alitawala Unyanyembe na alizaa watoto 7 nao ni (1.) Mtemi Isike mwana Kiyungi (2.) Mayole( 3.) Swetu Kalunga (4.) Kafululizya (5.)Sigimbi (6.) Nyamizi (7.)Sitta. Hawa nao wameendelea kuzaana mpaka leo wapo. Akiwamo Dada Nyanso na kina kaka Isike na wengine wapo Miwumba.
Kwa kifupi hivi ndivyo vilivyo vizazi vyetu vya pande mbili za Fundikira na Kiyungi wote Ni ndugu waliozaliwa na shina kuu Kaundi.

Mtemi SWETU
Ana historia nzuri sana, na ni mtu wa kukumbukwa sana alitawala Nsyepa mnamo mwaka 1800 utawala wake ulidumu kwa miaka 37, Ni mtemi aliyetawala toka akiwa kijana mpaka akazeeka na utemi wake. Mtemi Swetu alihamishia Ikulu ya Unyanyembe toka Nsyepa kwenda Itetemya na ndiye mwanzilishi wa jina Itetemya, hakuhama toka Nsyepa kuja Itetemya kwa kupenda bali alivamiwa na  jeshi la Wagaala akashindwa vita ndipo akakimbilia Itetemya kumpitia mwanawe Isale aka Fundikira ambaye wakati huo alikuwa Kigwa anajenga mji wake. Isale akakataa kukimbia na Baba yake badala yake akachukua jeshi la baba yake Mtemi Swetu akarudi Nsyepa kupigana na jeshi la Wagaala mpaka akashinda. Akamrudisha baba yake Nsyepa akaendelea na utawala wake.

Ndipo Mtemi Swetu akapata wazo la kujenga Ikulu mpya Itetemya ili iwe Ikulu ya akiba, ikitokea kashambuliwa na kupigwa na maadui akimbilie hapo Itetemya. Ulipofika mwaka 1830 akaamua kuhamia huko kabisa na miaka 7 baadae akafariki. Ndipo mwanaye Isale mwana Swetu aka Fundikira akatawala, huyu ndiye aliyewapiga Wagaala walipomshinda vita baba yake na kumrudisha akatawale Nsyepa.

Historia ya Utemi na kabila la Wanyanyembe!

MANGWILA

Hapo zamani za kale mnamo mwaka 1650 (Karne ya 16) mtu aitwae Mangwila alikuwa Mtaturu kwa kabila, kabila hili ni wenyeji wa Manyoni, Singida.

Huyu Mangwila shuhuli yake kubwa ilikuwa ni kuwinda Tembo. Siku moja akiwa na wapagazi wake waliondoka kambini Manyoni ambako wakati huo hapakuwa na mji bali pori kubwa na milima ambayo mpaka leo ipo. Walielekea Magharibi kwenye misitu ya Ukimbu.

Baada ya kufika kwenye misitu ya himaya ya Ukimbu waliomba kibali ruhusa ya kuwinda Tembo kwa Mtemi  aliyeitwa Malunkwi  maana wakati huo ilikuwa ni sheria mtu haruhusiwi kuwinda mpaka apewe ruhusa na watu wa kuongozana nao ili wamtoze ushuru wa meno atakayopata.

Baada ya kupewa kibali  alianza kazi ya kuwinda Tembo na akawa kila mara anarudi Utemini kwenda kulala na wapagazi wake.
Baada ya mwaka mmoja hivi akawa amezoeleka sana kwa Mtemi Malunkwi ndipo akaanzisha uhusianao wa kisiri na binti ya Mtemi  
Malunkwi ambaye alikuwa akiitwa Mloa.
Wakati huo ilikuwa ni marufuku kwa mtu wa kawaida kuwa na mahusiano au kumuoa mtoto wa Mtemi. Na ikibainika mtu amevunja amri hiyo hukumu yake huwa ni kifo tu. Kikawaida kwa wakati huo binti ya Mtemi aliozwa kwa watu wenye daraja kama Mtemi au  kama Waarabu au ndugu yake mwenye asili na damu ya kitemi, lakini si kwa watu wengine kwani wao walihesabika kama Watumwa tu, wasingeweza kuwaoa bwana zao.

Kitendo cha Mangwila kutembea na binti ya Mtemi Malunkwi hatimae kilisababisha binti yule kupata uja uzito. Ikabidi Mangwila akimbie na wapagazi wake wakaenda piga kambi katika misitu ya mbali na pale kwa Mtemi Malunkwi ambayo kwa sasa inajulikana kama Unyangwila. Mangwila na wapagazi wake walijificha katika misitu hiyo kwa mwaka mmoja hivi, watu wa Ukimbu walikuwa wanajua mahali alipojificha hivyo walikuwa wanamtembelea na kumpa habari mbali mbali za Mtemi Malunkwi na wao wakawa wanapewa nyama ya Tembo wakale ili wasiende kumwambia Mtemi Malunkwi walipojificha Mangwila na wapagazi wake.

Baadae wale watu walimpelekea habari Mangwila kuwa kuwa binti mfalme kajifungua mtoto wa kiume, baada ya kupata habari hizo Mangwila alituma ujumbe kwa Mtemi kuwa anaomba atume mali ili amgomboe mwanae, kwani sheria ilikuwa inaruhusu baada ya mtoto kuzaliwa hukumu ya kifo inasimamishwa na  Baba ataruhusiwa kumgomboa mwanae kwa kulipa meno ya tembo na kumchukua mwanae.
Mtemi alipopewa habari hizo akakubali na akamtoza Mangwila meno 10 ya Tembo, baada ya kupelekewa meno 10 akapewa mwanawe na kumpa jina la Nyembela. Lakini mama wa mtoto yule akakataa kumwacha mwanae achukuliwe peke yake, ndipo Mtemi Malunkwi akamwambaia Mangwila aongeze meno ya Tembo ili amuoze binti yake na aondoke nao mtoto na mama mtu. Baada ya kuwachukua mkewe na mtoto wakarejea kambini huko Unyangwila. Wakamlea yule mtoto mpaka akakua. Mangwila aliamua kuunda jeshi ili aweze kujilinda na maharamia ambao kazi yao ilikuwa ni kuwapora mali na meno ya Tembo wawindaji dhaifu. Nyembela akawa anaenda porini kuwinda wakiwa na jeshi lilioongozwa na baba yake Mangwila.

NYEMBELA
Baada ya miaka mingi kupita Mangwila alifariki kwa uzee na maradhi ambayo yalisadikika kuwa ni typhoid kutokana na maji waliyokunywa watu nyakati hizo hayakuwa safi na salama, ndipo mwanae Nyembela akarithi kazi yake ya uwindaji pamoja na jeshi la baba yake.
Baada ya miaka miwili kupita Nyembela alioa mke na akaendelea na kazi yake ya uwindaji.
Siku moja Nyembela alienda porini kuwinda na jeshi lake, walitembea kuelekea Magharibi walitembea kwa muda wa wiki nzima bila kupata Tembo hatimae wakajikuta wamefika mbali sana ndipo wakatokea kwenye mbuga kubwa sana na mbele ya mbuga hiyo kulikuwa na milima. Ghafla kwa mbali waliona Tembo wengi wakiwa wamekaa chini mmoja akiwa mkubwa sana kuliko wengine, ndipo Nyembela akajilaza chini na kuanza kutambaa kuelekea walipo Tembo huku akiwa ameshika mkuki wenye sumu, aliwasogelea mpaka karibu kabisa ndipo akamlenga yule Tembo mkubwa na kumrushia mkuki ukamchoma sikioni yule Tembo lakini badala ya kuanguka na kufa Tembo yule akaanza kumkimbiza Nyembela, naye akakimbia huku Tembo akimfuata kwa hasira mno, jeshi lake nalo likakimbia na kupanda juu ya miti.Nyembela akakimbilia milimani Tembo naye alizidi kumkimbiza Nyembela alipoukaribia  mlima akaona kwa chini ule mlima una uwazi kiasi cha futi tatu hivi basi akapenya pale na kupanda juu mlimani, yule Tembo kwa kuwa alikuwa mkubwa sana akashindwa kupenya pale penye uwazi akazunguka nyuma ya mlima kutafuta njia ya kupandia juu alipo Nyembela, kule nyuma yule Tembo akaanguka akafa bila Nyembela kujua. Kwa kuogopa kukutana na yule Tembo akaamua alale kule juu mlimani. Na jeshi lake likalala juu ya miti.

Kulipokucha akateremka chini akafuata nyayo za yule tembo mpaka akamkuta alipoangukia na kufa ndipo akapiga witi wale askari wake wakaja wakamng'oa meno kisha wakarudi nyumbani Unyangwila, waliporudi nyumbani wakawahadithia watu jinsi Nyembela alivyokoswa kuuawa na Tembo ndipo wazee wakashauri aende kwa mganga akapige ramli. Akapelekwa kwa mganga ndipo mganga wa jadi akamwambia "kilichokuponyesha si kingine bali ni mizimu" hivyo chukua ng'ombe wawili wote weusi urudi katika ile milima ukatambike kushukuru mizimu iliyokuponya na kifo. Nyembela akachukua ng'ombe akarudi milimani kutambika. Wakati wakifanya matambiko mke wa Nyembela alikuwa mja mzito waganga wakatabiri kuwa angezaa mtoto wa kiume na huyo mtoto atazaliwa na kukua kisha ataanzisha utawala wa kitemi wa eneo lile. Pia wakaamriwa kuwa huyo mtoto akizaliwa waende alipotokea bibi yake yaani mama yake Nyembela wakachukue ndezi ya utemi ili huyo mtoto atawale. 

KATWANGA

Baada ya muda mke wa Nyembela akazaa mtoto wa kiume akapewa jina Katwanga, yule bibi akarudi kwao akakuta baba yake Mtemi Malunkwi keshafariki na tayari palikuwa na Mtemi mwingine. akamsimulia yote yaliyotokea na akamuomba ampe ndezi naye akamkubalia akampa ndezi.

Mtemi Fundikira III akivalishwa ndezi 1957 baada ya kutawalishwa
Yule bibi akarudi Unyangwila na ndezi  na ndipo wakaamua kuhamia kule milimani na watu wa Unyangwila wakamfuata na kuanza kujenga mji katika eneo lile la milima na kupaita Unyanyembe. Katwanga alipofikisha umri wa miaka 15 alianza kujenga Ikulu kwenye eneo hilo akisaidiwa na wananchi wake na ilipomalizika mwaka 1727 (Karne ya 17) akatawazwa kuwa Mtemi
wa kwanza wa Unyanyembe na Ikulu yake aliita Nsyepa kumtukuza baba yake Nyembela aliyepona kuuawa na Tembo baada ya kupenya katika uwazi uliokuwepo mlimani na Tembo kushindwa kumpata. Ndipo jina la Nsyepa likavuma mpaka jina la Unyanyembe likabaki kuwa ni jina la ukoo wa kitemi na kuwa ndio jina la kabila la vizazi vyetu vyote mpaka leo, hivyo Wanyanyembe si jina la kujipa wala halikutokana na ubabe wa kivita.

Tuesday, April 12, 2011

Orodha ya Watemi wa Unyanyembe Ikulu ya Nsyepa
ORODHA YA WATEMI WA UNYANYEMBE KATIKA IKULU YA NSYEPA KUANZIA MWAKA 1727


No.
JINA
SEX
RULE
TO
YEARS
REASONS
OF DEATH
  1.
KATWANGA
M
1727
1737
9
Diseases
   2.
MPUTA
M
1737
1755
19
N/A
   3.
MPOPO
M
1755
1766
11
Died from Chicken pox
   4.
MTEMI KAUNDI
M
1766
1773
7
N/A
   5.
MTEMI SONSO aka NSEMAMILUNDI
F
1773
1780
7
Died from disease
   6.
MTEMI MMANYWA
M
1780
1790
10
Died from disease
   7.
MTEMI MGALULA
M
1790
1800
10
N/A


ORODHA YA WATEMI WA UNYANYEMBE KATIKA IKULU YA ITETEMIA

  8.
MTEMI SWETU
M
1800
1830 move 1837
37
Desease
  9.
MTEMI ISALE aka FUNDIKIRA
M
1837
1859
14
Desease
      10.
MTEMI MNWASELE
M
1859
1864
5
Removed from power
      11.
MTEMI KIYUNGI
M
1864
1885
21
Died from disease
      12.
MTEMI ISIKE MWANA KIYUNGI
M
1885
1893
8
Suicide
      13.
MTEMI NYANSO
F
1893
1896
3
Diseases
      14.
MTEMI KALUNDE MWANA GUMADI
F
1896
1917
22
N/A
      15.
MTEMI SAIDI FUNDIKIRA
M
1917
1928
11
Removed from power
      16.
MTEMI KIYUNGI (II) ISIKE
M
1928
1932
4
Desease
      17.
MTEMI ILAGILA MKASIWA
F
1932
1948
16
Died of NC
      18.
MTEMI FUNDIKIRA (II) NASSOR SAIDI
M
1948
1957
9
Shot himself
      19.
MTEMI FUNDIKIRA (III) ABDALAH  SAIDI
M
1957
2007
50
Died of NC
20. 20.
MTEMI MSAGATA NGULATI aka VANGWE MLAGAMAWI
M
2007
PRESENT
-
-