Wednesday, April 13, 2011

Tumbo la Kiyungi (Nsamama)

Mtemi Kiyungi baba yake aliitwa Msagata Mwana Mgalula, Kiyungi alizaliwa Uwemba (Zambia) .Wakati wa utawala wa Mtemi Fundikira ( I ) Msagata kazi yake ilikuwa kuwinda Tembo hivyo alikwenda Uwenba kuwinda Tembo, katika harakati zake zauwindaji huko Uwemba akampachika mimba binti ya Mtemi wa huko, kwa kuwa lilikuwa ni kosa kubwa  ilimbidi atoroke arudi nyumbani Unyanyembe, baada ya mwaka hivi zikaja habari kuwa binti ya Mtemi kajifungua mtoto wa kiume. Msagata akamwambia baba yake mdogo Mtemi Fundikira habari zile, Mtemi Fundikira akamwambia nenda pwani kauze meno ya Tembo ukirudi nitakupa mali ukamgomboe mwanao.

Msagata akaenda pwani kuuza meno ya tembo wakati anarudi akapata ugonjwa wa ndui akafa njiani. Ndipo Mtemi Fundikira  akamtuma mdogo wake Msagata aliyeitwa Msyama achukue mali aende akamgomboe yule mtoto kule Uwemba. Msyama akaenda kumgomboa akarudi na mtoto pamoja na mama yake, huko Uwemba mtoto yule alipewa jina la Nsamama. Na huku Nsyepa akapewa jina la Kiyungi. Mtemi Fundikira akafurahi sana kuona yule mtoto ameletwa, wakapiga lugaya pakachinjwa ng'ombe sherehe zilifanyika kwa siku 7, watu walikula na kucheza ngoma siku hizo zote.

Huyu Nsamama (Kiyungi) Baadae alitawala Unyanyembe na alizaa watoto 7 nao ni (1.) Mtemi Isike mwana Kiyungi (2.) Mayole( 3.) Swetu Kalunga (4.) Kafululizya (5.)Sigimbi (6.) Nyamizi (7.)Sitta. Hawa nao wameendelea kuzaana mpaka leo wapo. Akiwamo Dada Nyanso na kina kaka Isike na wengine wapo Miwumba.
Kwa kifupi hivi ndivyo vilivyo vizazi vyetu vya pande mbili za Fundikira na Kiyungi wote Ni ndugu waliozaliwa na shina kuu Kaundi.

Mtemi SWETU
Ana historia nzuri sana, na ni mtu wa kukumbukwa sana alitawala Nsyepa mnamo mwaka 1800 utawala wake ulidumu kwa miaka 37, Ni mtemi aliyetawala toka akiwa kijana mpaka akazeeka na utemi wake. Mtemi Swetu alihamishia Ikulu ya Unyanyembe toka Nsyepa kwenda Itetemya na ndiye mwanzilishi wa jina Itetemya, hakuhama toka Nsyepa kuja Itetemya kwa kupenda bali alivamiwa na  jeshi la Wagaala akashindwa vita ndipo akakimbilia Itetemya kumpitia mwanawe Isale aka Fundikira ambaye wakati huo alikuwa Kigwa anajenga mji wake. Isale akakataa kukimbia na Baba yake badala yake akachukua jeshi la baba yake Mtemi Swetu akarudi Nsyepa kupigana na jeshi la Wagaala mpaka akashinda. Akamrudisha baba yake Nsyepa akaendelea na utawala wake.

Ndipo Mtemi Swetu akapata wazo la kujenga Ikulu mpya Itetemya ili iwe Ikulu ya akiba, ikitokea kashambuliwa na kupigwa na maadui akimbilie hapo Itetemya. Ulipofika mwaka 1830 akaamua kuhamia huko kabisa na miaka 7 baadae akafariki. Ndipo mwanaye Isale mwana Swetu aka Fundikira akatawala, huyu ndiye aliyewapiga Wagaala walipomshinda vita baba yake na kumrudisha akatawale Nsyepa.

No comments:

Post a Comment