Wednesday, April 13, 2011

Historia ya Utemi na kabila la Wanyanyembe!

MANGWILA

Hapo zamani za kale mnamo mwaka 1650 (Karne ya 16) mtu aitwae Mangwila alikuwa Mtaturu kwa kabila, kabila hili ni wenyeji wa Manyoni, Singida.

Huyu Mangwila shuhuli yake kubwa ilikuwa ni kuwinda Tembo. Siku moja akiwa na wapagazi wake waliondoka kambini Manyoni ambako wakati huo hapakuwa na mji bali pori kubwa na milima ambayo mpaka leo ipo. Walielekea Magharibi kwenye misitu ya Ukimbu.

Baada ya kufika kwenye misitu ya himaya ya Ukimbu waliomba kibali ruhusa ya kuwinda Tembo kwa Mtemi  aliyeitwa Malunkwi  maana wakati huo ilikuwa ni sheria mtu haruhusiwi kuwinda mpaka apewe ruhusa na watu wa kuongozana nao ili wamtoze ushuru wa meno atakayopata.

Baada ya kupewa kibali  alianza kazi ya kuwinda Tembo na akawa kila mara anarudi Utemini kwenda kulala na wapagazi wake.
Baada ya mwaka mmoja hivi akawa amezoeleka sana kwa Mtemi Malunkwi ndipo akaanzisha uhusianao wa kisiri na binti ya Mtemi  
Malunkwi ambaye alikuwa akiitwa Mloa.
Wakati huo ilikuwa ni marufuku kwa mtu wa kawaida kuwa na mahusiano au kumuoa mtoto wa Mtemi. Na ikibainika mtu amevunja amri hiyo hukumu yake huwa ni kifo tu. Kikawaida kwa wakati huo binti ya Mtemi aliozwa kwa watu wenye daraja kama Mtemi au  kama Waarabu au ndugu yake mwenye asili na damu ya kitemi, lakini si kwa watu wengine kwani wao walihesabika kama Watumwa tu, wasingeweza kuwaoa bwana zao.

Kitendo cha Mangwila kutembea na binti ya Mtemi Malunkwi hatimae kilisababisha binti yule kupata uja uzito. Ikabidi Mangwila akimbie na wapagazi wake wakaenda piga kambi katika misitu ya mbali na pale kwa Mtemi Malunkwi ambayo kwa sasa inajulikana kama Unyangwila. Mangwila na wapagazi wake walijificha katika misitu hiyo kwa mwaka mmoja hivi, watu wa Ukimbu walikuwa wanajua mahali alipojificha hivyo walikuwa wanamtembelea na kumpa habari mbali mbali za Mtemi Malunkwi na wao wakawa wanapewa nyama ya Tembo wakale ili wasiende kumwambia Mtemi Malunkwi walipojificha Mangwila na wapagazi wake.

Baadae wale watu walimpelekea habari Mangwila kuwa kuwa binti mfalme kajifungua mtoto wa kiume, baada ya kupata habari hizo Mangwila alituma ujumbe kwa Mtemi kuwa anaomba atume mali ili amgomboe mwanae, kwani sheria ilikuwa inaruhusu baada ya mtoto kuzaliwa hukumu ya kifo inasimamishwa na  Baba ataruhusiwa kumgomboa mwanae kwa kulipa meno ya tembo na kumchukua mwanae.
Mtemi alipopewa habari hizo akakubali na akamtoza Mangwila meno 10 ya Tembo, baada ya kupelekewa meno 10 akapewa mwanawe na kumpa jina la Nyembela. Lakini mama wa mtoto yule akakataa kumwacha mwanae achukuliwe peke yake, ndipo Mtemi Malunkwi akamwambaia Mangwila aongeze meno ya Tembo ili amuoze binti yake na aondoke nao mtoto na mama mtu. Baada ya kuwachukua mkewe na mtoto wakarejea kambini huko Unyangwila. Wakamlea yule mtoto mpaka akakua. Mangwila aliamua kuunda jeshi ili aweze kujilinda na maharamia ambao kazi yao ilikuwa ni kuwapora mali na meno ya Tembo wawindaji dhaifu. Nyembela akawa anaenda porini kuwinda wakiwa na jeshi lilioongozwa na baba yake Mangwila.

NYEMBELA
Baada ya miaka mingi kupita Mangwila alifariki kwa uzee na maradhi ambayo yalisadikika kuwa ni typhoid kutokana na maji waliyokunywa watu nyakati hizo hayakuwa safi na salama, ndipo mwanae Nyembela akarithi kazi yake ya uwindaji pamoja na jeshi la baba yake.
Baada ya miaka miwili kupita Nyembela alioa mke na akaendelea na kazi yake ya uwindaji.
Siku moja Nyembela alienda porini kuwinda na jeshi lake, walitembea kuelekea Magharibi walitembea kwa muda wa wiki nzima bila kupata Tembo hatimae wakajikuta wamefika mbali sana ndipo wakatokea kwenye mbuga kubwa sana na mbele ya mbuga hiyo kulikuwa na milima. Ghafla kwa mbali waliona Tembo wengi wakiwa wamekaa chini mmoja akiwa mkubwa sana kuliko wengine, ndipo Nyembela akajilaza chini na kuanza kutambaa kuelekea walipo Tembo huku akiwa ameshika mkuki wenye sumu, aliwasogelea mpaka karibu kabisa ndipo akamlenga yule Tembo mkubwa na kumrushia mkuki ukamchoma sikioni yule Tembo lakini badala ya kuanguka na kufa Tembo yule akaanza kumkimbiza Nyembela, naye akakimbia huku Tembo akimfuata kwa hasira mno, jeshi lake nalo likakimbia na kupanda juu ya miti.Nyembela akakimbilia milimani Tembo naye alizidi kumkimbiza Nyembela alipoukaribia  mlima akaona kwa chini ule mlima una uwazi kiasi cha futi tatu hivi basi akapenya pale na kupanda juu mlimani, yule Tembo kwa kuwa alikuwa mkubwa sana akashindwa kupenya pale penye uwazi akazunguka nyuma ya mlima kutafuta njia ya kupandia juu alipo Nyembela, kule nyuma yule Tembo akaanguka akafa bila Nyembela kujua. Kwa kuogopa kukutana na yule Tembo akaamua alale kule juu mlimani. Na jeshi lake likalala juu ya miti.

Kulipokucha akateremka chini akafuata nyayo za yule tembo mpaka akamkuta alipoangukia na kufa ndipo akapiga witi wale askari wake wakaja wakamng'oa meno kisha wakarudi nyumbani Unyangwila, waliporudi nyumbani wakawahadithia watu jinsi Nyembela alivyokoswa kuuawa na Tembo ndipo wazee wakashauri aende kwa mganga akapige ramli. Akapelekwa kwa mganga ndipo mganga wa jadi akamwambia "kilichokuponyesha si kingine bali ni mizimu" hivyo chukua ng'ombe wawili wote weusi urudi katika ile milima ukatambike kushukuru mizimu iliyokuponya na kifo. Nyembela akachukua ng'ombe akarudi milimani kutambika. Wakati wakifanya matambiko mke wa Nyembela alikuwa mja mzito waganga wakatabiri kuwa angezaa mtoto wa kiume na huyo mtoto atazaliwa na kukua kisha ataanzisha utawala wa kitemi wa eneo lile. Pia wakaamriwa kuwa huyo mtoto akizaliwa waende alipotokea bibi yake yaani mama yake Nyembela wakachukue ndezi ya utemi ili huyo mtoto atawale. 

KATWANGA

Baada ya muda mke wa Nyembela akazaa mtoto wa kiume akapewa jina Katwanga, yule bibi akarudi kwao akakuta baba yake Mtemi Malunkwi keshafariki na tayari palikuwa na Mtemi mwingine. akamsimulia yote yaliyotokea na akamuomba ampe ndezi naye akamkubalia akampa ndezi.

Mtemi Fundikira III akivalishwa ndezi 1957 baada ya kutawalishwa
Yule bibi akarudi Unyangwila na ndezi  na ndipo wakaamua kuhamia kule milimani na watu wa Unyangwila wakamfuata na kuanza kujenga mji katika eneo lile la milima na kupaita Unyanyembe. Katwanga alipofikisha umri wa miaka 15 alianza kujenga Ikulu kwenye eneo hilo akisaidiwa na wananchi wake na ilipomalizika mwaka 1727 (Karne ya 17) akatawazwa kuwa Mtemi
wa kwanza wa Unyanyembe na Ikulu yake aliita Nsyepa kumtukuza baba yake Nyembela aliyepona kuuawa na Tembo baada ya kupenya katika uwazi uliokuwepo mlimani na Tembo kushindwa kumpata. Ndipo jina la Nsyepa likavuma mpaka jina la Unyanyembe likabaki kuwa ni jina la ukoo wa kitemi na kuwa ndio jina la kabila la vizazi vyetu vyote mpaka leo, hivyo Wanyanyembe si jina la kujipa wala halikutokana na ubabe wa kivita.

No comments:

Post a Comment