Thursday, April 14, 2011

Mtemi Isale aka Fundikira (I)

MTEMI ISALE aka FUNDIKIRA

Alikuwa Mtemi wa pili kutawala katika Ikulu ya Itetemya, alitawala mpaka akazeeka kiasi kwamba wabaya wake na watu wasiompenda wakawa wanamafanyia njama ili wamuue ili atawale mtu mwingine.

CHANZO CHA JINA FUNDIKIRA

Miongoni mwa watu waliomchoka Mtemi Isale alikuwa ndugu yake mmoja akiitwa Mkelemi, huyu Mkelemi alikuwa mtoto wa Kiwisuka mwana Sambwe, yeye alikuwa akiishi eneo ambalo kwa sasa linaitwa Tuli. Akawa anazungumza wazi wazi "Huyu Mtemi mbona anachelewa kufa, na sisi tutatawala lini?, akaongeza ipo siku nitaenda kumsabahi na ndipo nitamchoma mkuki afe"

Habari hizo zikaenea mpaka zikamfikia mwenyewe Mtemi Isale. Mtemi akaona bora asipuuze, akawaita wazee wanikulu wazijadili zile habari, wamchukulie hatua gani huyo Mkelemi. Baada ya mjadala mrefu wakakubaliana wampelekee  jeshi likampige afe. Wakati wanapanga mikakati hiyo ya kumpelekea jeshi alikuwepo mtoto wa Mtemi Mmanywa, yeye alipinga wazo la kumpelekea jeshi mtu mmoja akawaambia "niachieni mimi nitamuua kwa mkono wangu"

Wazee na Mtemi wakakubali wakamuachia yeye akamuue Mkelemi. Nkosi alikuwa akiishi Migwenhwe hivyo akatuma ujumbe kwa Mkelemi kuwa anamualika aende kwake akamtembelee. Mkelemi alikubali na ilipofika siku hiyo Nkosi akachimba shimo la duara na ndani ya shimo akachomeka mikuki na miti yenye ncha kali huku ikiwa imeangalia juu. Akachukuaa miti akaitandika juu ya shimo lile akatandaza majani kisha akafunika na udongo na juu yake akaweka kiti. Ilipofika saa 5 hivi Mkelemi akawasili kwa Nkosi, akampokea na kumkaribisha katika kiti alichokiandaa na Mkelemi alipokaa tu akatumbukia na kuchomwa na mikuki na miti iliyokuwamo mle shimoni akawa analia huku akisema "Nkosi wambulaga"  akimaanisha Nkosi umeniua. Nkosi akamjibu "Nkali nene wakuwala uwayawako msava veve ulikova kumwulaga Mtemi wakusumla kinani? akimaamisha Nkosi akaona Mkelemi anachelewa kufa akachomoa mkuki akainama na kumchoma Mkelemi lakini kumbe Mkelemi nae alichomoa kisu na kunyoosha mkono juu kile kisu kikamchoma Nkosi tumboni na yeye akaangukia humo shimoni akafa kwa utumbo wake ulimwagika kutokana na jeraha la kisu cha Mkelemi. Mke wa Nkosi akaanguka chini na kuanza kulia na kupiga ukelele uuuwi winulaga akimaanisha jamani wamemuua. Watu wakaja wakawatoa toka mle shimoni. Nkosi akawa ashakufa lakini Mkelemi akawa bado hajafa. wakawabeba kwenye machela mbili wakawapeleka Ikulu kwa Mtemi. Wakamsimulia Mtemi yaliyotokea, Mtemi akawaambia "huyu Mkelemi mpelekeni kwake na huyu Nkosi tumzike.

Watu wakambeba wakimrudisha nyumbani kwake njiani huku akivuja sana damu Mkelemi akawaambia "mwemweye ntulinasuhe, wale wtu wakamshusha chini akasema " mpagi minzi nang'we"
wakafuata maji kwenye malambo wakampa akanywa alipomaliza kunywa akafa.Wakabeba maiti mpaka nyumbani kwake, kesho yake wakazika, tokea siku hiyo eneo hilo likaitwa Tuli mpaka leo eneo hilo linaitwa hivyo.

Baada ya siku 40  Mtemi Isale akawaambia watu leteni nguo za Mkelemi na Nkosi walipoleta nguo zao akawaambia sikilizeni hizi nguo nitazichukua mimi kwa sababu hawa Mkelemi na Nkosi wameuana kwa ajili yangu akasema kwa kinyamwezi navakundikila Nkosi na Mkelemi akimaanisha nawafunika Mkelemi na Nkosi. Tangu siku hiyo mtemi akawa anaitwa ikundikila na jina hilo likabaki mpaka hii leo na ndio asili ya jina la Fundikira.

3 comments:

  1. Asante sana sana kwa Ku document historia yetu.

    ReplyDelete
  2. Daah kumbe jina LA Mmanywa nilopewa linameanzia uku babu Said tunakuomba uendeleze hii historia

    ReplyDelete